Wednesday, June 21, 2017

WADAU WA SEKTA YA MBEGU WAHIMIZWA KUWEKEZA ZAIDI KUZALISHA MBEGU ZA MBOGAMBOGA HAPA NCHINI.Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi  Mhe. Charles John Tizeba, amewaagiza wataalamu wa Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi kwa kushirikisha Wadau wa Tasnia ya Mbegu kuandaa mkakati wa kusaidia uzalishaji wa kutosha wa mbegu  za mazao ya  mbogamboga.  Amesema hayo katika Warsha ya Wadau wa Mbegu iliyofanyika  katika Hoteli ya Mount Meru Arusha. 

Mhe. Waziri amesema, nchi kwa sasa inaupungufu mkubwa wa mbegu za mbogamboga ingawa uzalishaji wa mazao hayo umekuwa ukichangia kwa kiasi kikubwa katika Uchumi na pato la Taifa.
Amesema, Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi kupitia Sheria ya Mbegu Na.18 ya Mwaka 2003 imefanya maboresho makubwa ya kuwezesha mbegu za Kilimo kupatikana kwa wingi hapa nchini. Kupitia marekebisho ya Sheria na Kanuni, kwa sasa, muda wa majaribio ya mbegu mpya umepunguzwa kutoka miaka mitatu na sasa majaribio hayo ni msimu mmoja tu hususan kwa mbegu zinazotoka nchi zenye makubaliano ya udhibiti wa Ubora wa mbegu na Tanzania ikiwemo nchi za SADC.

Aidha , Mhe. Waziri ameiagiza Taasisi ya Udhibiti wa Mbegu nchini (TOSCI) kusimamia kwa karibu Sheria ya Mbegu ili kusaidia kuwalinda wakulima dhidi ya wafanyabiashara wasiowaaminifu ambao wanauza mbegu zisizo na ubora  (Mbegu feki).
Awali, aliwaeleza Wadau wa Mbegu nchini kuwa nchi ina  upungufu wa mbegu bora kutokana na uwekezaji mdogo kwenye tasnia ya Mbegu.

Aliwajulisha Wadau kuwa ili kuwezesha sekta binafsi kuzalisha mbegu zilizogunduliwa na vituo vya Utafiti vya Serikali, Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi imetoa Waraka maalumu unaoweka utaratibu wa jinsi ya sekta binafsi itakavyoweza kupata kibali cha kutumia mbegu hizo za umma.
Amewaahidi Wadau kuimarisha Maabara ya Taasisi ya Udhibiti wa Mbegu (TOSCI) ili iweze kutekeleza vyema mikataba ya Kikanda na Kimataifa kuhusu masuala ya ubora  wa mbegu. Alisema, Wizara itatoa kiasi cha Dola za Kimarekani  13,000 kwa ajili ya kuwezesha Maabara ya TOSCI kupata ithibati (accreditation) ya Shirika la Kimataifa la Mbegu (ISTA). Ithibati hiyo itasaidia mbegu zinazozalishwa nchini ziweze kuuzwa bila kikwazo nje ya Tanzania.
Amewataka Wadau wa Mbegu kutumia fursa ya ardhi yenye rutuba kuanzisha na kuendeleza mashamba ya mbegu. Pia, aliwaasa washirikiane na Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) ili kupata maeneo ya kuzalisha mbegu kwa makubaliano maalumu.

Ameongelea fursa kubwa iliyopo kwenye kilimo kwa kuondolewa kwa tozo kwenye maeneo mbalimbali kwenye sekta ya kilimo. Alisema, takriban tozo 80 zimeondolewa kwa Wizara ya Kilimo tu ukiondoa zile zilizokuwa zikisimamiwa na Wizara nyingine.

Aliwapongeza wafanyabishara wa mbegu kwa kuwa kiungo muhimu kwenye maendeleo ya tasnia ya mbegu. Aliahidi Wizara yake kuyafanyia Kazi yale ambayo yataazimiwa na Wadau wa mbegu.

Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi Mheshimiwa Mhandisi Dk. Charles Tizeba

Friday, June 9, 2017

Maonesho ya Kilimo na Sherehe za Wakulima –Nane Nane Mwaka 2017

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi anatangazia umma kuwa Maonesho ya Kilimo na Sherehe za Wakulima – Nane Nane mwaka 2017, ngazi ya Ki-Taifa zitaadhimishwa katika Uwanja wa Maonesho ya Kilimo wa Ngongo, Manispaa ya Lindi. Maandalizi na maonesho hayo yanaratibiwa na Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na uongozi wa Mikoa ya Lindi na Mtwara. 

Uratibu wa maonesho ya mwaka huu ngazi ya Ki-Taifa unafanywa na Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi kwa kuwa Taasisi ya Kilimo Tanzania (TASO) iliyokuwa inaratibu maandalizi na maonesho ya Wakulima (Nane Nane) miaka ya nyuma imefutiwa usajili wake mwezi Mei 2017. Washiriki wa maonesho ya kilimo na sherehe za Ki-Taifa wawasiliane moja kwa moja na Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi au Sekretarieti za Mikoa ya Lindi na Mtwara. 

Aidha, maadhimisho ya Ki-Kanda yatafanyika katika  viwanja vya maonesho ya John Mwakangale –Mbeya; Mwalimu J.K. Nyerere –Morogoro; Themi – Arusha; Nzuguni -  Dodoma; Nyahongolo – Mwanza; na Fatuma Mwassa - Tabora. Maandalizi na maonesho ya  Ki-Kanda yanaratibiwa na uongozi wa  mikoa husika. Washiriki wa maadhimisho ya Ki-Kanda wanatakiwa kuwasiliana na Sekretarieti za Mikoa husika ili kupata maelekezo na taratibu zingine za ushiriki. 

Hivyo kuanzia sasa utaratibu wa maandalizi na maonesho ya sherehe za wakulima (Nane Nane) ni kama ulivyotolewa katika tangazo hili. Maelezo zaidi kuhusu maonesho ya kilimo na sherehe za wakulima yataendelea kutolewa kupitia njia zifuatazo:-
www.tzagriculture.blogspot.com;
www.twitter.com/tzagriculture
WOTE MNAKARIBISHWA

Monday, June 5, 2017

Wakulima Wavutiwa na Mbegu Bora za Mpunga
                 
Wakulima mkoani morogoro wamevutiwa na mbegu mpya za mpunga ambazo zinastawi nchi kavu,zinachukua muda mfupi kukomaa na zina mavuno mengi.
Ufanisi wa mbegu hizo ulionekana  katika mashamba darasa ya mpunga katika vijiji vya Kisaki,Tawa ,Msonge, Tawa, Kiloka, Dala na Mtamba katika Halmashauri ya Mororogoro vijijini ambapo wakulima wa maeneo hayo walifanya majaribio ya aina nne za mbegu za mpunga.
Wakiongea kwa nyakati tofauti wakati wa Siku ya Mkulima iliyofanyika katika  kijiji cha Mtamba hivi karibuni na kuhudhuriwa na viongozi wa  ngazi ya Mkoa Wilaya pamoja na Vijiji  wakulima hao wamesema, mbegu aina ya Nerika 1, Nerika 2, Nerika 4 na Nerika 7 zinapendwa na wakulima kutokana na uwingi wake wa mazao kwa ekari pamoja na muda mfupi wa kukomaa
Hamis Mfaume ni mkulima wa kiongozi wa kijiji cha Kisaki Morogoro Vijijini anasema majaribio ya mbegu waliyafanya katika mashamba manne tofauti ambapo imeonekana dhahiri kuwa mbegu hizo zina ufanisi mkubwa
tulifanya majaribio katika mashamba  manne tulikopanda  aina nne za mbegu ambazo zilikuwa ni Nerika 1  inachukua kati ya siku 95-100, na hutoa kilo 1800 kwa ekari moja. Nerika 2 huchukua siku 90-95 toka kupandwa hadi kuvunwa na hutoa kilo 1600 kwa ekari moja, wakati Nerika 7 inatoa kilo 2000 kwa ekari moja na huchukua siku kati ya 95 mpaka 100’. Alisema hamisi mfaume
Aidha Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) Dk. Firmin Mizambwa amewataka wakulima  kuchagua aina moja au mbili ya mbegu hizo ambazo wanazipenda ili waendelee kuzizalisha katika mashamba yao  na pia kuwa na  mpunga unaofanana katika eneo moja na kuvutia soko.
Aidha Dk. Mizambwa aliwataka wakulima hao viongozi kuendelea kutoa elimu kwa wakulima wengine ili kuongeza uzalishaji na kuimarisha usalama wa chackula nchini.